Huku Kenya inapojiandaa kuandaa fainali ya kuwania kombe la Mataifa Bingwa Afrika mwaka 2027 (AFCON 2027), ujenzi wa uwanja wa michezo wa Kimataifa wa Raila Odinga, awali ukijulikana kama Talanta, unakaribia kukamilika.
Uwanja huo ulio pewa jina Raila Odinga kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya hayati Raila Odinga, una uwezo wa kuwakimu mashabiki 60,000.
Kwenye ukurasa wa X, Katibu katika Wizara ya Uslama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema ujenzi wa uwanja huo uko katika hatua za mwisho mwisho, huku mwanakandarasi akianza shughuli ya kuweka viti, vifaa vya mawasiliano, taa, na vifaa vya ICT.
“Uwanja huo utakuwa na chumba cha kuhifadhi maji na paa lililo na uwezo wa kuvuna maji ya mvua, na kuitumia upya katika unyunyizaji maji kwa uwanja,” alisema Katibu huyo.
Kenya inajizatiti kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa wakati, huku ikijiandaa kuandaa fainali hizo pamoja na Tanzania na Uganda mwaka 2027.
Wizara ya Usalama wa Taifa imetekeleza jukumu muhimu katika kuongoza operesheni za asasi mbalimbali za ujenzi wa uwanja huo kuhakikisha unaafikia viwango vinavyohitajika.