Waakilishi pekee wa Afrika waliosalia katika Kombe la Dunia Morocco, waterejea uwanjani leo Alhamisi Julai 9, kwa mechi ya kwanza ya robo fainali katika uwanja wa Boston nchini Marekani.
Robo fainali hiyo ambayo itakuwa mechi nambari 97, katika kipute cha mwaka huu inachezwa baada ya mapumziko ya siku moja.
Ufaransa maarufu The Blues, wanajivunia kutoshindwa wala kutoka sare kwenye fainali za mwaka huu wakishinda Senegal,Norway na Iraq na kuongoza kundi I, kwa pointi 9.
Katika awamu ya 32 bora Ufaransa chini ya ukufunzi wa Didier Deschamps, iliwabandua Uswidi mabao 3-1, na hatimaye kuibwaga Paraguay bao moja bila katika hatua ya 16 bora.

Atlas Lions ya Morocco nao walimaliza nafasi ya pili kundi D kwa alama 7 ,wakitoka sare na Brazil, kabla ya kuwanyuka Scotland na Haiti.
Katika raundi ya 32 bora Morocco, iliwatimua Uholanzi penati 3-2, kufuatia sare ya 1-1,na hatimaye kuwalabua wenyeji Canada 3-0, kwenye 16 bora.
Ni mara ya pili mtawalia kwa Morocco, chini ya ukufunzi wa Mohamed Ouahbi, kucheza robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kumaliza ya nne miaka minne iliyopita.
Aidha,Simba Atlas ndio timu ya kwanza ya Afrika kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia mtawalia.
Mechi ya leo kati Ufaransa na Morocco, itakuwa ya sita baina ya timu hizo mbili,Ufaransa wakishinda tatu na nyingine mbili kumalizikia sare.
Mechi pekee ambavyo timu hizo zimekutana katika Kombe la Dunia, ilikuwa semi fainali ya mwaka 2022 nchini Qatar, Wafaransa wakishinda 2-0.