Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, amesema serikali imejitolea kuimarisha Taasisi za Umma na utoaji huduma hapa nchini.
Ruku alisema kupitia mageuzi yanayoendelea, serikali inajizatiti kuboresha utumishi wa umma ambao unazingatia uwajibikaji na unaoshughulikia changamoto ibuka.
Akizungumza Jumatatu wakati wa kuadhimisha siku ya Utumishi wa Umma barani Afrika, waziri huyo alidokeza kuwa wizara yake sasa inaangazia kushughulikia mahitaji ya wananchi na kutimiza matarajio ya Wakenya wanaotafuta huduma katika taasisi na asasi za umma.
“Ikiwa tumejitolea kushindana na mataifa bora zaidi duniani, utoaji wetu wa huduma unapaswa kuimarika na kufikia viwango vya mataifa hayo,” alisema waziri Ruku.
“ikiwa tunataka kuwa kama Singapore au Korea Kusini, watumishi wa umma na wananchi lazima waangazie utoaji huduma kwa kila saa, badala ya kufika tu afisini,” aliongeza Ruku.
Mkutano huo uliandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Jijini Nairobi.