Maafisa wa Kupambana na Ufisadi (EACC), wamewakamata maafisa wawili wa Halmashauri ya Kukusanya Ushuru (KRA), kwa madai ya kuitisha hongo ya shilingi milioni tatu kutoka kwa mlipa ushuru.
Washukiwa hao Faith Gathoni Njoroge na Tyson Marango Owuor, wanaohudumu katika afisi za KRA eneo la Upper Hill, walitiwa nguvuni kufuatia malalamishi kutolewa dhidi yao kwamba waliitisha hongo ili wavuruge taarifa za ushuru za thamani ya shilingi milioni 4.5.
Kulingana na EACC, wawili hao walikamatwa walipokuwa wakipokea shilingi 900,000 kama sehemu ya hongo ya shilingi milioni tatu.
Fedha hizo zilipatikana wakati wa operesheni hiyo, huku washukiwa hao wakizuiliwa katika Makao Makuu ya EACC, uchunguzi ukiendelea.
Wawili hao wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya kupokea mlungula, chini ya sheria ya kukabiliana na ulaji rushwa ya mwaka 2016.