Rais William Ruto leo Ijumaa amefanya mabadiliko kwa baadhi ya maafisa wa ngazi za juu katika Vikosi vya Ulinzi nchini (KDF).
Kwenye mabadiliko hayo Meja Jenerali John Maiso Nkoimo ameteuliwa kuwa Naibu kamanda wa jeshi la nchi kavu, akichukua nafasi ya Meja Jenerali Mohamed Nur Hassan ambaye anaelekea kwenye likizo ya kustaafu.
Brigedia William Kamoiro amepandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali, huku Brigedia Peter Kipketer Limo akipandishwa madaraka na kuwa Meja Jenerali katika wadhifa wa afisa msaidizi wa majeshi ya ulinzi (maafisa na usafirishaji), akichukua nafasi ya Meja Jenerali Edward Rugendo ambaye ameteuliwa kusimamia kitengo cha huduma za maslahi ya vikosi vya ulinzi.
Kipindi cha kuhudumu cha Meja Jenerali Paul Owuor Otieno, kimeongezwa kwa mwaka mmoja.
Brigedia Dkt. Francis Njoroge Kuria amepandishwa cheo na kuchukua wadhifa wa Meja Jenerali, akichukua wadhifa wa kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu.
Kanali Peter Karigi Kariuki naye amepandishwa cheo na kuwa Brigedia huku akiteuliwa katibu katika chuo cha kitaifa cha Jeshi la Ulinzi.
Mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha uongozi na uendeshaji shughuli katika vikosi vya Ulinzi (KDF).