Ruto: Kenya ina mafuta ya kutosha

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kwamba nchi hii ina mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yake. 

Kadhalika Ruto amesifia mpangokazi wa G2G ambao amesema umesaidia kuhakikisha usambazaji thabiti wa mafuta nchini licha ya mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

Mgogoro huo umevuruga usambazaji wa mafuta na kusababisha bei ya bidhaa hiyo kuongezeka duniani kote.

“Kupitia mpangokazi wa usambazaji wa G2G, tumepata usambazaji thabiti wa mafuta licha ya kuvurugika kwa mtungo wa usambazaji duniani, na kuhakikisha upatikanaji usiotatizika wa mafuta kote nchini,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia taifa kutoka Ikulu ya Mombasa leo Ijumaa asubuhi.

Amesema mpango huo umekuwa nguzo muhimu kuhakikisha usambazaji thabiti wa mafuta nchini hata wakati majanga kama vile linaloshuhudiwa duniani kwa sasa.

Ruto alipuuzilia mbali miito ya kuondoa ushuru kwenye bidhaa za petroli akisema hatua kama hiyo itaathiri mno utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara na ufadhili wa masomo bila kuisaza sekta ya afya miongoni mwa zingine.

Alielezea imani kwamba janga linaloshuhudiwa kwa sasa litamalizika na hali ya kawaida kurejea.

 

 

Share This Article