Timu ya soka ya shule ya upili ya wavulana ya Tenwek kutoka kaunti ya Bomet, leo ijumaa imefuzu katika mashindano ya kitaifa kwa mara ya kwanza baada ya kuilaza shule ya Menengai kutoka kaunti ya Nakuru mabao matatu kwa mawili katika fainali ya mashindano ya shule za upili ya eneo la Bonde la Ufa iliyosakatwa ugani Ole Ntimama mjini Narok.
Taarifa hii yenye mshangao kwa wafuasi wa mashindano hayo imejiri baada ya miamba wa mkoa huo na mabingwa mara sita wa kitaifa – St. Antony ya mjini Kitale kubanduliwa na Menengai hapo jana katika nusu fainali na kuifanya kusakata mchuano wa nafasi ya tatu ambapo waliinyofoa Kapsoit magoli tisa bila jibu.
Kwenye upande wa vipusa, St. Joseph kutoka Kitale ilijikatia tiketi ya kitaifa kufuatia ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Nasokol.
Katika raga ya wachezaji saba kila upande, wavula wa Laiser Hill na warembo wa Itigo ndio mabingwa wapya kufuatia ushindi wa alama 25 na 19 kwa sufuri dhidi ya St. Antony na St.Joseph mtawalia.
Mashindano ya kitaifa yataandaliwa mjini Thika baadaye mwezi huu.
Taarifa ya Boniface Mutsotso