Uhispania almaarufu La Roja watashuka uwanjani Los Angeles kukabiliana na Red Devils wa Ubelgiji kuanzia saa nne usiku Ijumaa kuwania tiketi ya nusu fainali.
Robo fainali hiyo itashirikisha timu hizo ambazo zimekuwa zikifanya vyema zikiwa hazijapoteza mechi katika kipute cha Kombe la Dunia.
Ublegiji iliongoza kundi G kwa pointi 5, wakitoka sare dhidi ya Misri na Iran na hatimaye kuinyuka New Zealand.
Katika awamu ya 32 bora, Ubelgiji iliwabwaga Senegal 3-2 katika muda wa ziada na hatimaye kuwabandua wenyeji Marekani magoli 4-1 katika awamu ya 16.

Uhispania ambayo ndiyo timu pekee haijafungwa bao katika Kombe la Dunia mwaka huu waliongoza kundi H kwa alama 7, wakitoka sare dhidi ya Cape Verde kabla ya kuzilemea Saudi Arabia na Uruguay.
Katika raundi ya 32, Uhispania iliwabwaga Austria 3-0 na kisha kuwatuma nyumbani Ureno kwa kuwapiga 1-0 katika awamu ya 16 .
Uhispania na Ubelgiji zitakutana Ijumaa kwa mechi ya 14, Uhispania wakishinda saba, sare tatu na Ubelgiji wakashinda 3.

Katika Kombe la Dunia, miamba hao wa Ulaya watakuwa wakipambana kwa mara ya tisa, Uhispania wakishinda 5, Ubelgiji wakaibukia mara moja na mechi mbili kuishia sare.
Mshindi wa mechi hiyo atakumbana na Ufaransa kwenye nusu fainali ya kwanza Jumanne ijayo, Julai 14 katika uwanja wa Dallas.