Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefariki dunia leo, Septemba 7, 2026, Zanzibar, akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.
Taarifa za kifo chake zimetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi.
Hafidh na Dkt. Samia walifunga ndoa mwaka 1978 na walijaliwa watoto wanne, wavulana watatu na msichana mmoja. Kitaaluma, Hafidh alikuwa mtaalamu wa kilimo na aliwahi kuwa mtumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta hiyo.
Baada ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2021, kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli, Hafidh akawa mume wa kwanza wa Rais wa Tanzania, nafasi inayojulikana kwa Kiingereza kama ‘First Gentleman’.
Miongoni mwa watoto wake ni Wanu Hafidh Ameir, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye mwaka 2025 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Katika maisha yake, Hafidh aliishi kwa kiasi kikubwa maisha ya faragha na hakujihusisha hadharani na shughuli za kisiasa, licha ya kuwa mume wa Rais wa nchi.