Rais Ruto: Adui wa Afrika Mashariki ni umaskini na ukosefu wa ajira

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais wa Kenya William Ruto.

Rais wa Kenya William Ruto ametoa wito kwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushirikiana pamoja kuimarisha utangamano, ili kufanikisha maendeleo katika kanda hii.

Ruto ambaye alizungumza alipohutubia Bunge la Tanzania Jijini Dodoma siku ya Jumanne, alitoa wito wa juhudi za pamoja katika kukabiliana na jinamizi la ukosefu wa ajira, umaskini na ukosefu wa maendeleo.

“Tuko na maadui wengi. Maadui wetu si Wakenya wala Watanzania, bali ni ukosefu wa ajira, umaskini na maendeleo,” alisema Rais Ruto.

kiongozi huyo wa Kenya alihimiza umuhimu wa kuboresha Jumuiya ya Afrika Mashariki bila ubaguzi wa kitaifa, akitaja kuwa “kile ambacho ni kizuri kwa Kenya, ni kuzuri kwa Tanzania,”.

“Haijalishi rasilimali inapatikana upande upi wa mpaka, la muhimu ni ikiwa inaimarisha ufanisi wetu wa pamoja,” alidokeza kiongozi huyo wa Kenya.

Aidha, alisema Kenya na Tanzania hutegemeana pakubwa huku biashara kati ya nchi hizo mbili ikifika dola milioni 860 mwaka 2025, akidokeza kuwa nchi hizo zinalenga kufikisha uwekezaji huo hadi dola bilioni 1 mwaka 2026.

“Tuna mpaka wa pamoja wa takriban kilomita 800, kutoka bahari hindi Lunga Lunga hadi Horohoro, Kilimanjaro, na kutoka Serengeti hadi ziwa Victoria,” aliongeza Rais Ruto.

Rais William Ruto ndiye Rais wa pili kutoka Kenya kuhutubia Bunge la Tanzania, baada ya Rais Mstaafu hayati Daniel Arap Moi kulihutubia mwaka 2002.

Share This Article