Mshukiwa wa mauaji ahukumiwa kifo Kisumu

Aidha, mahakama pia ilifahamishwa kwamba Otieno alijaribu kumuua dada yake Monica Atieno ambaye aliyetoroka na kunusurika kifo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Mshukiwa wa mauaji ahukumiwa kifo Kisumu.

Mahakama Kuu ya Kisumu, imemhukumu kifo mwananume aliyepatikana na hatia ya kuwaua watu wanne akiwemo mwana wake wa kiume, mke wake, mjomba wake na jirani.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mnamo Februari 24, 2024 katika Kijiji cha Nyangoma, kaunti ndogo ya Muhoroni kaunti ya Kisumu, Shem Akuku Otieno almaarufu Daddy, alitekeleza mauaji ya wanne hao, kabla ya kutoroka na kisha kujisalimisha kwa polisi.

Awali alikuwa amekanusha mashtaka hayo, lakini baadaye alikiri mauaji ya mwana wake wa kiume Joseph Omua Akuku mwenye umri wa miaka saba kwa kumkata kwa panga, mke wake Emily Adhiambo mwenye umri wa miaka 26, mjomba wake Thomas Odula Nyameche na jirani Mary Kuya Otieno mwenye umri wa miaka 56 na ambaye alikuwa akiugua.

“Nataka kufahamisha mahakama kwamba niliwaua watu hao wanne. Nakiri mashtaka ya kuwaua wanne hao,” alisema Otieno, licha ya kufahamishwa kuwa hukumu ya kosa la mauaji ni kifo.

Aidha, mahakama pia ilifahamishwa kwamba Otieno alijaribu kumuua dada yake Monica Atieno ambaye aliyetoroka na kunusurika kifo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na kiongozi wa mashtaka Mercy Mutheu Muema, uliwasilisha ushahidi wa kutosha kumhusisha Otieno na mauaji hayo, huku Jaji wa Mahakama Kuu ya Kisumu Justice Joe M. Omido akitoa hukumu ya kifo dhidi ya Otieno kuambatana na sehemu ya 203 na 204 ya katiba ya Kenya.

Share This Article