Rais William Ruto, amesema Kenya itaendelea kufanya kazi na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, kwa lengo la kuimarisha ushughulikiaji wa dharura katika kanda hii.
Aliyasema hayo Jumatatu aliposhiriki mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu Jagan Chapagain katika Ikulu ya Nairobi.
“Nilimhakikishia Chapagain kuwa Kenya itaendelea kufanya kazi na Shirika la Msalaba Mwekundu kushughulikia dharura,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alimfahamisha Katibu Mkuu huyo kuhusu ajenda ya mageuzi ya Kenya, hususan katika uvunaji wa maji, uhifadhi wa maji na unyunyizaji mashamba maji kupitia hazina ya taifa ya miundombinu.
“Miradi hiyo itaimarisha uzalishaji na kuboresha utoshelevu wa chakula wa taifa hili,” alidokeza kiongozi huyo wa taifa.
Aidha, Ruto aliishukuru Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kuendelea kutekeleza mipango ya kibinadamu nchini Kenya na katika kanda hii.