Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema serikali jumuishi inafanya kazi kwa bidii ya mchwa kuhakikisha wagombea wake wanaibuka washindi katika chaguzi ndogo zijazo.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Novemba 27 imepanga kufanya chaguzi ndogo 24 katika maeneo mbalimbali kote nchini.
Prof. Kindiki amesema muungano wa Kenya Kwanza na chama cha ODM zimekubaliana kuunga mkono wagombea wao katika chaguzi hizo.
Amewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi na kuwapigia kura wagombea wa vyama hivyo.
Naibu Rais aliyasema hayo leo Ijumaa katika mkutano wa uwezeshaji kiuchumi katika eneo bunge la Kasipul uliofanyika katika uwanja wa Kituo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Sikri huko Oyugis, kaunti ya Homa Bay.
“Sote tumekubaliana kufanya kazi pamoja na kuunga mkono kikamilifu wagombea wetu wa serikali jumuishi katika chaguzi ndogo zijazo. Makubaliano yaliyotiwa saini na Rais Ruto na aliyekuwa kiongozi wa ODM marehemu Raila Odinga yameturuhusu kusimama kidete na wagombea wanaoungwa mkono na vyama vyetu,” alisema Prof. Kindiki.

Chaguzi hizo zimepangwa kufanywa katika maeneo bunge ya Kasipul, Ugunja, Malava, Mbeere North, Banisa na Magarini, miongoni mwa mengine.
Prof. Kindiki alisema wagombea wa ODM huko Kasipul, Ugunja na Magarini wanaungwa mkono kikamilifu na serikali jumuishi.

Hali ni yiyo hiyo kwa wagombea wa UDA katika maeneo ya Malava, Banisa, Mbeere North and Baringo.
Katika baadhi ya maeneo, ushindani mkali unatarajiwa kushuhudiwa, mathalan, katika eneo bunge la Malava.
Huko, mgombea wa chama cha DAP-K Seth Panyako atatoana jasho na mgombea wa chama tawala cha UDA David Ndakwa huku ikisemekana ushindani kati ya wawili hao umekuwa mkali zaidi.
DCP imetangaza kuondolewa kwa mgombea wake katika eneo la Malava na sasa inaunga mkono Panyako wa DAP-K.
Katika eneo bunge la Kasipul, mgombea wa ODM, Boyd Were, anapeperusha bendera ya chama hicho, na anakabiliwa na upinzani kutoka mgombea huru Philip Aroko na wagombea wengine wawili.
“Sisi ni timu moja na hapa Kasipul tunamuunga mkono kikamilifu mgombea wa ODM. Pia tunafanya hivyo huko Ugunja na Magarani na pia katika maeneo yote ambapo wagombea wa UDA wanapeperusha bendera yetu,” aliongeza Naibu Rais.
Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, ambaye pia ni mwenyekiti wa kitaifa wa ODM, alisema hawatajitenga na makubaliano hayo na kuahidi kuunga mkono kikamilifu wagombea wa serikali jumuishi.
“Katika chaguzi ndogo zijazo, tunaunga mkono wagombea wote wa serikali jumuishi kwa sababu tumekubaliana kwamba tutawaunga mkono wagombea wetu katika chaguzi hizo,” alisema Gavana Wanga.
Wanga akiongeza kuwa chama cha ODM kitasalia serikalini kama kilivyoelekezwa na kiongozi wake aliyeondoka, marehemu Raila Odinga.