Raia wawili wa India waliotekwa nyara waokolewa, washukiwa watatu wakamatwa

Wakati wa operesheni hiyo, polisi walipata simu za waathiriwa hao zilizokuwa zimefichwa kichakani takriban kilomita mbili kutoka kwa nyumba hiyo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Raia wawili wa India waliokuwa wametekwa nyara waokolewa.

Raia wawili wa India waliotekwa nyara muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), wameokolewa, huku washukiwa watatu wa utekaji nyara huo raia wa Pakistan wakikamatwa.

Uchunguzi wa Polisi umebainisha kuwa raia hao wawili wa India Sandeep Sandeep na Ishwar Singh, waliwasili katika uwanja wa JKIA saa nane alasiri, na walipokewa na wanaume wawili kabla ya kuabiri gari aina ya Nissan note na kuondoka.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kupitia ukurasa wa X, ilisema kuwa uchunguzi uliwapeleka maafisa hao hadi kwenye nyumba moja mtaani Tumaini, Nkoroi, kaunti ya  Kajiado, ambako waliwapata raia hao wa India waliokuwa wametoweka.

Raia watatu wa Pakistan waliopatikana kwenye nyumba hiyo Shahzad Haroon, Tariq Muhammad Muneeb na Hassan Waqar, walikamatwa papo hapo, huku ikibainika kuwa washukiwa hao tayari walikuwa wamewasiliana na familia ya waathiriwa nchini India na kuitisha dola 32,000 ili kuwaachilia huru mateka hao.

Wakati wa operesheni hiyo, polisi walipata simu za waathiriwa hao zilizokuwa zimefichwa kichakani takriban kilomita mbili kutoka kwa nyumba hiyo.

Washukiwa hao watatu wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article