Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC, inawaongoza wadau mbalimbali kushiriki Kongamano la Kitaifa la Amani linalofanyika jijini Nairobi.
Maafisa kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Idara ya Mahakama, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na sekta ya usalama ni miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo la siku mbili lililong’oa nanga leo Jumatatu.
Lengo la kongamano hilo lenye kaulimbiu “Amani Kenya”, likiwa kujadiliana mbinu bora za kudumisha amani kwa kuhakikisha hata punje ya vurugu haishuhudiwi nchini wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Kongamano hili siyo mkutano wa kawaida tu. Ni jukwaa kazi la kutathmini, kuratibu na kuelezea dhamira ili Wakenya waweze kufurahia uchaguzi mkuu wa amani usiokuwa na vurugu,” alisema Dkt. Daniel Giti, Afisa Mkuu Mtendaji wa NCIC wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox akitoa wito kwa wadau wote daima kuheshimu sheria kwa manufaa ya nchi.
“Pamoja, tunaweza tukabadilisha mwelekeo kutoka njia hatari na uharibifu na badala yake kuchagua utawala wa sheria, ushirikiano, uwajibikaji na amani. Uchaguzi utakuja na kwenda, lakini Kenya itasalia,” alisema Cox.
Wanasiasa nao walitakiwa kuchunga ndimi zao la sivyo wanaweza kuwa tishio kwa utangamano wa kitaifa.
“Lazima tuwakumbushe wanasiasa wetu kwamba hakuna mwanasiasa ambaye ni mkubwa kuliko Kenya, na hakuna chama cha kisiasa ambacho ni kikubwa kuliko Kenya. Kenya daima inakuja kwanza,” alisema Askofu Geoffrey Njuguna.
Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli alilalamikia visa vya uhuni ambavyo vimeshuhudiwa katika mikutano ya kisiasa katika siku za hivi karibuni akisema watakaopatikana watachukuliwa hatua kali.