Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu amekata rufaa dhidi ya kifungo chake cha miaka 12 gerezani au faini ya shilingi milioni 53.5 iliyotolewa na Mahakama ya Kupambana na Ufisadi, baada ya kupatikana na hatia katika sakata ya utoaji zabuni ya shilingi milioni 588.
Waititu ambaye alipatikana na hatia Alhamisi iliyopita na Hakimu Mkuu Thomas Nzioki, alihukumiwa kwa kutoa kandarasi ya kukarabati barabara kaunti ya Kiambu katika mwaka wa kifedha wa 2017-2018 , bila kufuata taratibu za kisheria.
Mahakama hiyo pia ilimzuia Waititu kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa muda wa miaka 10.
Washtakiwa wenzake, akiwemo mkewe Susan Wangari, pia walihukumiwa, huku Wangari akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Testimony Enterprises Charles Chege, alitozwa faini ya shilingi milioni 295, huku mhandisi wa barabara Lucas Wahinya akitozwa faini ya shilingi milioni 21.
Baada ya hukumu hiyo, Waititu, kupitia kwa wakili wake John Swaka, aliomba kusindikizwa hadi hospitalini, lakini hakimu aliamua kwamba wakuu wa magereza wangeshughulikia hali yake.