Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa watatu waliohusishwa na visa vya wizi wa kimabavu na ubakaji katika kijiji cha Ichinga, kaunti ndogo ya Mumias katika kaunti ya Kakamega.
Kulingana na ripoti ya polisi katika kituo cha polisi cha Kabras, washukiwa hao Michael Natili Khasatsili mwenye umri wa miaka 20, Tyson Maikuva aliye na umri wa miaka 18 na Brian Omondi Opondo mwenye umri wa miaka 32, wanadaiwa waliwavamia waathiriwa wawili wa kike ambao ni wahudumu wa afya, walipokuwa wakitoka kazini Februari 10, 2025.
Katika kisa hicho kilichotokea katika kituo cha kibiashara cha Ekero, washukiwa hao waliwapeleka waathiriwa hadi katika sehemu iliyojificha na kuwapora simu zao za mkononi na kuwaitisha kwa lazima nambari za siri za simu hizo, kabla ya kuwabaka.
Baada ya kutendewa unyama huo, waathiriwa hao walitafuta huduma za matibabu katika kituo cha afya cha St. Mary’s kabla ya kutakiwa kutafuta matibabu katika hospitali ya Level IV ya Mumias.
Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI, walianzisha operesheni ya kuwasaka washukiwa hao na juhudi zao zilizaa matunda, walipowafumania washukiwa hao katika maficho yao Februari 15, 2025.
Maafisa hao walipata moja ya simu za rununu zilizoibwa kutoka kwa waathiria aina ya Samsung Galaxy A05.
Watatu hao walifikishwa katika mahakama ya Butali ambako walizuiliwa kwa siku tano, kuwapa polisi fursa ya kukamilisha uchunguzi.
Kesi hiyo itatajwa Februari 26, 2025.