Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Nape Nnauye amesema serikali ya nchi hiyo inajitahidi kuunda mfumo mzuri ambao utatambua na kulinda ubunifu wa vijana nchini humo.
Huku akikiri kwamba wengi wa vijana hulazimika kusajili ubunifu wao kwenye nchi jirani zilizo na sera bora za kulinda biashara changa za ubunifu, Nape alisema wameshafanya vikao na wamekubaliana na wadau mbali mbali ndani na nje ya Tanzania wameweka msingi wa kubuni sera hizo na wako tayari kwa hatua itakayofuata.
Anahisi mfumo huo ukianzishwa unaweza kusaidia vijana hao kuvutia wawekezaji nchini Tanzania kupitia ubunifu wao.
“Kwa muda kidogo Sekta hii imekuwa haina mfumo mzuri wa kisheria wa kuratibu ubunifu wa Ki-TEHAMA hapa nchini na matokeo yake tunao Vijana wa Kitanzania ambao wanafanya ubunifu lakini wanalazimika kwenda Nchi jirani kusajili ubunifu wao na kuufanya ubunifu wao ufanye kazi.” alisema waziri huyo.
Alitoa mfano wa kijana kwa jina Benjamin Fernandes mwanzilishi wa mfumo wa kutuma na kupokea pesa unaofahamika kama “NALA”.
Waziri Nape aliyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari baada ya kufunga Kikao na Wadau Kujadili Ushirikiano wa Maendeleo Juu ya Sera ya Kampuni Changa za TEHAMA nchini Tanzania, Jijini Dar es Salaam.