Rais Ruto ataka pande husika kukomesha mapigano nchini DRC

Ruto aliongoza kikao cha EAC na SADC cha kujadili hali ya DRC nchini Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amelitaka kundi la waasi la M23 nchini Congo lililotwaa udhibiti wa jiji la Goma Mashariki mwa DRC likomeshe mapigano na kudhibiti maeneo mengine.

Akizungumza katika kikao cha pamoja cha Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC nchini Tanzania, Rais Ruto alilitaka jeshi la DRC nalo lisitekeleze mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Ruto alisisitiza haja ya kujitolea kikamilifu kuafikia amani, maendeleo na ushirikiano endelevu nchini DRC na katika eneo zima.

Kiongozi wa nchi alilalamika kwamba wengi wamefariki na vitega uchumi vya wengi kuharibiwa hatua ambayo imetumbukiza wakazi wengi katika wimbi la kutokuwa na uhakika kuhusu maisha yao.

Aliongeza kusema kwamba DRC ilipoteza fursa ya kuharakisha ukuaji na maendeleo ndiposa kujitolea kikamilifu kwa amani na haki ni muhimu sasa.

Wakati huo huo Rais Ruto alisema kwamba mzozo wa DRC ni changamoto, tete, wa muda mrefu na unahusisha watu kadhaa ambao wanafuatilia maslahi tofauti.

Alisisiriza haja ya viongozi wa EAC na SADC kuendeleza kutoka kwa mazuri yaliyoafikiwa na mafunzo yaliyotokana na michakato ya amani ya Luanda na Nairobi.

Vile vile Rais William Ruto alitaka kwamba makundi yanayozozana nchini DRC yakomeshe vita ili kuhakikisha hali haiwi mbaya zaidi.

Ruto ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa kikao hicho cha Tanzania pamoja na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, aliwataka viongozi wa nchi wanachama wa EAC na SADC wajitolee kikamilifu kwa mchakato wa amani.

Kulingana naye, hali ya DRC inahusu jamii nzima ya kimataifa kwa sababu kadhaa huku akiomba jamii hiyo ya kimataifa isaidie katika juhudi za kurejesha amani nchini DRC.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *