Rais wa kwanza wa Namibia Sam Nujoma afariki

Rais Nujoma anaripotiwa kufariki usiku wa manane akipokea matibabu kwenye hospitali moja jijini Windhoek.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa kwanza wa taifa la Namibia Sam Nujoma amefariki. Haya ni kulingana na tangazo lililotolewa leo Jumapili Februari 9, 2025 na Rais wa sasa Nangolo Mbumba.

Rais Nangolo Mbumba katika taarifa alisema kwamba Rais wa zamani Sam Shafiishuna Nujoma, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 95, usiku wa manane Februari 8, 2025, akiendelea kupokea matibabu jijini Windhoek.

Nujoma amelazwa hospitalini kwa muda wa wiki tatu zilizopita kutokana na ugonjwa ambao haukutajwa lakini juhudu za madaktari hazikufanikiwa.

Rais Mbumba amemtaja marehemu Nujoma kuwa mmoja wa wazaliwa wa nchi ya Namibia ambao ni hodari zaidi na uongozi wake ulikuwa muhimu katika kupigania uhuru wa nchi hiyo na kuanzishwa kwa Namibia huru.

Aliangazia kujitolea kwa Nujoma katika kuhamasisha na kuleta umoja nchini Namibia na kuiongoza nchi hiyo kutoka kwa nyakati ngumu hadi ilipopata uhuru mwezi Machi mwaka 1990.

“Wakati wa maombolezi ya kitaifa, tunafaa kutiwa moyo na uongozi wa kipekee wa Rais Nujoma na mchango wake mkubwa kwa taifa.” Alisema Rais Mbumba katika taarifa.

Alitoa rambirambi zake kwa mkewe Nujoma Kovambo Nujoma na kwa familia za Nujoma na Kondombolo.

Serikali ya Namibia inatarajiwa kutangaza maelekezo zaidi kuhusu maombolezi ya kitaifa na mipango ya mazishi ya kiongozi huyo wa kwanza wakati wowote kuanzia sasa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *