Jeshi la Sudan larejesha udhibiti wa sehemu kubwa ya jiji la Khartoum

Jeshi hilo limekuwa likipambana na kundi la wapiganaji la RSF ambalo lilinyakua udhibiti wa maeneo kadhaa nchini Sudan.

Marion Bosire
2 Min Read

Jeshi la Sudan limetangaza kwamba limerejesha usimamizi wa eneo kubwa la Khartoum Kaskazini linapoendeleza mashambulizi yanayolenga kuchukua usimamizi wa jiji hilo kuu kutoka kwa wapiganaji wa RSF.

Jeshi hilo ambalo limekuwa likipigana na RSF tangu Aprili 2023, limeweza kurejesha maeneo kadhaa ya jiji la Khartoum na maeneo ya karibu katika siku za hivi maajuzi.

Jana Jumamosi jeshi hilo lilitangaza kwamba limetwaa usimamizi wa wilaya ya Kafouri, ambayo ni muhimu katika eneo la Khartoum Kaskazini baada ya kusukuma wapiganaji wa RSF hadi eneo la Bahri.

Kafouri ni mojawapo ya wilaya zenye utajiri mkubwa nchini Sudan na imekuwa chini ya usimamizi wa RSF na ina nyumba ambazo zinamilikiwa na viongozi wakuu wa RSF kama vile Abdel Rahim Daglo kakake kamanda msaidizi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo.

Ijumaa jeshi hilo lilitangaza pia kwamba limetwaa usimamizi waeneo la Abu Quta katika jimbo la Gezira ambalo liko Kaskazini Magharibi kutoka kwa RSF.

Msemaji wa jeshi la Sudan Nabil Abdullah alisema katika taarifa kwamba wanajeshi waliondoa wanachama waliokuwa wamesalia wa RSF kutoka Kafouri na maeneo yaliyo umbali wa kilomita 15 kuelekea mashariki mwa Sharq El Nil.

Alhamisi duru za jeshi hilo ziliarifu shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi walikuwa wanaelekea katikati mwa Khartoum, huku walioshuhudia wakisema kulikuwa na mapigano na milipuko kusini mwa Khartoum.

Wanajeshi sasa wanadhibiti miji yote ya jimbo la Gezira isipokuwa mji wa Giad ulioko kaskazini pamoja na vijiji vilivyo ndani ya umbali wa kilomita 50 kaskazini mwa Khartoum.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *