Wizara ya Afya yahimiza maandalizi kabla ya mvua ya El Niño

Katibu Mary Muthoni, amezitaka kaunti na idara nyingine za afya kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, chanjo na hatua za kukabiliana na milipuko.

Marion Bosire
2 Min Read
Mary Muthoni - Katibu katika Wizara ya Afya

Wizara ya Afya imetoa wito wa kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari za kiafya zinazohusishwa na mvua ya El Niño inayotarajiwa kunyesha.

Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni, amezitaka kaunti na idara nyingine za afya kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, chanjo na hatua za kukabiliana na milipuko.

Akizungumza katika kikao cha kila wiki cha usimamizi, Muthoni alisema Kenya inapaswa kuwa macho dhidi ya mpox, surua, polio, pamoja na Ebola katika maeneo ya kuingilia nchini.

Kufikia Septemba 12, 2026, Kenya ilikuwa imerekodi visa 1,309 vilivyothibitishwa vya mpox na vifo 19 katika kaunti 40. Nchi pia ilikuwa imeripoti visa 469 vya surua, kikiwemo kifo kimoja.

Kisa kimoja cha virusi vya polio aina ya 2 vilivyobadilika kutoka chanjo pia kimethibitishwa Dadaab, Kaunti ya Garissa.

Muthoni pia amezitaka mamlaka za afya kujiandaa kukabiliana na magonjwa yanayoenezwa kupitia maji na wadudu, ambayo yanaweza kuongezeka kutokana na mvua ya El Niño inayotarajiwa.

Alizitaka kaunti kuimarisha maandalizi, utoaji wa chanjo, ushirikishaji wa jamii na ulinzi wa wahudumu wa afya.

Aidha, ametoa wito wa hatua zilizoratibiwa, kurugenzi na vitengo mbalimbali ili kusaidia kinga ya afya ya umma, huduma za afya ya msingi, usalama wa afya na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu huyo pia amewataka wadau kuunga mkono maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Umma wa Kenya, KEPHIC 2026, utakaofanyika Oktoba 27 hadi 29, 2026.

Share This Article