MCK – Wanahabari walindwe, wasishambuliwe

Kufikia sasa, jumla ya wanahabari 18 na madereva wasiopungua 2 wameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. 

Martin Mwanje
2 Min Read
David Omwoyo - Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK

Baraza la Vyombo vya Habari nchini, MCK limeshutumu kile ambacho limetaja kuwa ongezeko la mashambulizi dhidi ya wanahabari wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. 

Wa hivi punde kushambuliwa na wahuni ni wanahabari 8 waliokuwa wakifuatilia mkutano wa vuguvugu la Linda Mwananchi katika kaunti ya Homa Bay jana Jumapili.

“Baraza lina mashaka makubwa kuhusu mashambulizi yasiyowahi kutokea dhidi ya wanahabari nchini kote katika wiki za hivi karibuni ambayo yamesababisha majeraha, uharibifu wa vifaa, na unyanyasaji mitandaoni unaofanywa na maafisa wa usalama, wahuni, na wafuasi wa vyama vya kisiasa, huku hatua ndogo zikichukuliwa na mamlaka husika,” MCK ililalama kwenye taarifa ya Mkurugenzi wa Mafunzo ya Uanahabari, Victor Bwire.

“Kukosa kuchukua hatua ni hatari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Licha ya sheria za Kenya na mikataba ya kimataifa inayohitaji mamlaka kuhakikisha mazingira salama kwa wanahabari, usalama wao bado haupo.”

MCK sasa inatoa wito kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Inspekta Mkuu wa Polisi kuwachukua hatua haraka watu wanaotekeleza mashambulizi dhidi ya wanahabari.

Kwa mujibu wa baraza hilo, kufikia sasa, jumla ya wanahabari 18 na madereva wasiopungua 2 wamedhulumiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Chama cha Wahariri nchini, KEG na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International ni miongoni mwa wealioshutumu mashambulizi dhidi ya wanahabari nchini.

 

 

Share This Article