Polisi hatimaye wamesitisha kimya saa kadhaa baada ya vurugu kutokea wakati wa mkutano wa vuguvugu la Linda Mwananchi katika kaunti ya Homa Bay jana Jumapili.
Kwenye taarifa, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kupitia kwa msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS Muchiri Nyaga anasema washukiwa 37 wamekamatwa kufikia sasa kuhusiana na vurugu hizo.
“NPS bado inamsaka Oliver Jaoko almaarufu ‘Olivetti’, ambaye kwa sasa ameenda mafichoni, na inamtaka kujisalimisha kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu ili kusaidia katika uchunguzi unaoendelea,” alisema Muchiri.
“Operesheni za kumkamata na wengine wote waliohusika kwenye vurugu hizo zinaendelea.”
Wengine wanaosakwa ni pamoja na waratibu, wawezeshaji na wafadhili wa vurugu hizo kwa lengo la kuwawajibisha.
Kwa mujibu wa Muchiri, waliokamatwa walipatikana wakiwa na silaha hatari ikiwa ni pamoja na mapanga, kamba, visu, marungu, nguzo za chuma na tochi.
NPS ikielezea kuwa wanahabari kadhaa na pia maafisa wa polisi walijeruhiwa wakati wa patashika hiyo huku magari 5 ya polisi yakiharibiwa.
Baraza la vyombo vya habari linasema jumla ya wanahabari 8 walijeruhiwa wakati wa ghasia zilizotokea Homa Bay jana Jumapili.
Viongozi wa Linda Mwananchi wamewanyoshea kidole cha lawama baadhi ya wanasiasa wa kaunti ya Homa Bay kwa kufadhili vurugu hizo huku maafisa wa polisi wakilaumiwa kwa utepetevu.
Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC pia imelaani vikali ghasia hizo ikiapa kuwawajibisha wahusika.
Kwenye taarifa, mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Kepha Omae ametoa wito wa uvumilivu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 akionya kuwa vurugu zinazoshuhudiwa kwa sasa ni tishio kwa usalama wa taifa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.