Maandalizi yanoga ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu ukinukia

Rais William Ruto ataongoza hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho kitakachojengwa na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote Jumatano wiki ijayo.

Martin Mwanje
2 Min Read
Picha kwa hisani ya Radio Kaya

Zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta huko Lamu kuanza kwa kishindo, maandalizi yamepamba moto. 

Kamishna wa kaunti ya Lamu Stephen Sangolo anasema maandalizi ya hafla ya uwekaji jiwe la msingi ya kiwanda hicho kinachohusishwa na mwekezaji bilionea wa Nigeria Aliko Dangote yameshika kasi.

Rais William Ruto ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho Septemba 30 katika hafla ambayo pia itahudhuriwa na Marais kadhaa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa sasa, serikali inafanya mikutano na washikadau mbalimbali kuhusu mradi huo wakati ikikusanya maoni ya wakazi kuuhusu.

Akizungumza wakati kongamano la ushiriki wa umma, Sangolo alisema serikali imefanya mashauriano na viongozu wa Lamu na makundi mbalimbali ya jamii kuhakikisha mashaka yote ya wakazi yanashughulikiwa.

Wakati huohuo, viongozi wa jamii katika kaunti ya Lamu wanaendelea kuisihi serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha mradi huo unawafaidi wakazi hasa kupitia kubuni nafasi za ajira, biashara na kiuchumi.

Awali, Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni mradi wa kupigiwa mfano utakaofungua uchumi wa eneo la Lamu na Pwani kwa jumla kwa kubuni takriban nafasi za ajira 50,000.

Akizungumza wakati wa mkutano wa maandalizi ya mwisho ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda hicho uliofanyika mtaani Karen jijini Nairobi mapema wiki hii, Prof. Kindiki alisema mradi huo utapiga jeki jitihada za Kenya za kuwa nchi iliyostawi zaidi kiviwanda.

“Huu ni mradi muhimu zaidi kwa nchi yetu na kwa kanda hii. Unaenda kutoa huduma za petrokemikali na shughuli za kiviwanda katika eneo hili,” alisema Prof. Kindiki.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa na Dangote aliyekutana na Rais Ruto Jumatatu wiki hii pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA jijini New York nchini Marekani.

Share This Article