Msajili Mkuu wa zamani wa Ardhi wa Kilifi Felix Mecha Nyakundi, mkewe Stellah Nyaboke Otwori na kampuni zinazohusishwa na familia ya msajili huyo wameagizwa kurejesha mali na fedha ambayo thamani yake ni shilingi milioni 426.8.
Wote hao waliagizwa na Mahakama Kuu kurejesha mali hiyo kwa serikali baada ya kubainika ilipatikana kwa njia isiyoeleweka.
Kwenye uamuzi wake, Jaji B.M. Musyoki wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi alisema Nyakundi na wenzake walishindwa kuiridhisha mahakama namna walivyojipatia mali hiyo ikilinganishwa na vyanzo vyao halali vya mapato.
Kesi dhidi yao iliwasilishwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC.
Mali walizoagizwa kurejesha ni pamoja na shilingi milioni 233.5 zilizohifadhiwa kwenye akaunti za benki na MPesa, viwanja na mashamba yenye kima cha shilingi milioni 177.1 yaliyopo katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Kilifi na magari matatu yenye thamani ya shilingi milioni 11.9.
EACC imeimarisha msako dhidi ya maafisa wa serikali waliojizolea mali na mamilioni ya pesa zinazoshukiwa kupatikana kwa njia ya ulaghai.