Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kahawa West jijini Nairobi wameimarisha msako dhidi ya utengenezaji na usambazaji wa pombe haramu.
Msako huo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuikinga jamii dhidi ya bidhaa zinazohatarisha maisha na usalama wake.
Maafisa walifanya operesheni kali katika maeneo ya Soweto na Saa Mbaya, ikilenga nyumba zinazoshukiwa kutumiwa kutengeneza pombe na kuuza mihadarati.
Wakati wa msako huo, lita 2,600 za pombe ya kangara na lita 120 za pombe ya chang’aa zilinaswa na kumwagwa huku vifaa vinavyotumiwa katika utengenezaji wa pombe hiyo pia vikiharibiwa.
Huduma ya Taifa ya Polisi imeahidi kuimarisha zaidi misako ya kukabiliana na utengenezaji wa pombe haramu inayohatarisha maisha ya binadamu.