Uganda waishika mateka Tunisia mechi za kufuzu AFCON

Botswana na Libya waliambulia sare ya 2-2 katika mechi nyingine ya kufuzu mjini Tripoli.

Dismas Otuke
1 Min Read

Uganda Cranes walitoka nyuma na kulazimisha sare ya bao moja dhidi ya Tunisia katika mechi ya kundi H kufuzu kwa fainali za mwaka ujao za AFCON iliyoandaliwa mjini Radès, Alhamisi usiku.

Adem Arous aliwaweka mbele wenyeji Carthage Eagles katika dakika ya 12 lakini Uganda Cranes wakasawazisha kunako dakika ya 68 kupitia kwa Rogers Mato.

Botswana na Libya waliambulia sare ya 2-2 katika mechi nyingine ya kufuzu mjini Tripoli.

Katika kundi E, Chui wa DRC wakiwa nyumbani waliipakata Equitorial Guinea mabao 2-0 huku Zimbabwe wakitoka nyuma mabao 2 na kuwagutusha Sierra Leone 3-2 mjini El Jadida Morocco.

Mabingwa mara tano Cameroon almaarufu Indomitable Lions waliititiga Comoros 3-1 katika kundi G wakati Namibia ikiwanyoa Congo bao moja kwa nunge katika pambano jingine.

Mauritania wakiwa nyumbani waliiparuza Jamhuri ya Afrika ya Kati magoli 3-1 katika kundi F.

Kundini C, tembo wa Ivory Coast waliwabwaga mabingwa mara nne wa AFCON Ghana mabao 2-0.

Share This Article