Wabunge wanaohudhuria Mkutano wa 69 wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPC) mjini Cape Town nchini Afrika Kusini wamezishutumu serikali zao husika kwa kushindwa kuangazia changamoto zinazowakumba walemavu.
Hii ni licha ya kuwepo sheria na sera zilizodhamiria kulinda haki zao. Nao walielezea lalama zao wakati wa kikao cha kujadili namna mabunge yao yanavyoweza kutunga sheria ya ujumuishaji wa walemavu.

Wabunge kutoka mataifa mbalimbali ya Jumuiya ya Madola walielezea kufadhaika kwao na kile walichokitaja kuwa utekelezaji mbovu wa sheria za walemavu, kutengwa katika ajira na fursa za kibiashara na kutopata huduma muhimu ipasavyo.
Kulingana nao, serikali zao kwa kiwango kikubwa zimeshindwa kutekeleza mipangokazi ya sheria na sera iliyokusudiwa kulinda maslahi ya walemavu.
Walidai kushindwa huko kumewafungulia wengi milango ya umaskini, ubaguzi na kutengwa katika jamii.
Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi, anayehudhuria mkutano huo, alisema Kenya imepiga hatua katika kutunga sheria za kuwasaidia walemavu lakini utekelezaji wake unasalia kuwa changamoto.
Aliongeza kuwa baadhi ya maafisa wa serikali wanaendelea kupuuza sheria hizo bila kuchukuliwa hatua.
“Tumeshuhudia baadhi ya visa ambapo walemavu wamekosa kuteuliwa katika nyadhifa kuu serikalini. Hatua kama hizo zinaua ari ya ujumuishaji,” alilalama Wanyonyi.
“Tuna walemavu wanaotimiza vigezo vya kuhudumu serikalini lakini hawateuliwi.”
Wabunge wa Afrika Kusini, wakiongozwa na Tsehofatso Chauke, walikubaliana na kauli hizo, wakiishutumu serikali yao kwa kushindwa kutekeleza sheria madhubuti ya kuangazia mahitaji ya walemavu.
Aidha, waliishutumu serikali hiyo kwa kushindwa kutekeleza sera zilizopo kwa manufaa ya walemavu.