Kundli la mwisho la Maafisa wa Polisi wa Kenya, limeondoka nchini Haiti na kurejea nyumbani, hatua inayoashiria kukamilika kwa kipindi cha vikosi vya usalama vya kimataifa kudumisha amani katika taifa hilo la Amerika ya Kaskazini.
Maafisa hao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumanne jioni, wakiwa wameandamana na Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mshauri wa Usalama wa Taifa Joseph Boinett miongoni mwa maafisa wakuu wa usalama.
Akizungumza kuhusu kikosi cha Kenya kilichoshiriki katika operesheni hiyo ya kukabiliana na magenge yaliyokuwa yameshikilia maeneo kadhaa nchini Haiti, Murkomen alisema polisi wa Kenya walipata ufanisi wa kupigiwa mfano, hususan baada ya kutwaa maeneo muhimu kama vile uwanja wa ndege, bandari na mapito makuu ya usafiri.
“Wakishirikiana kwa karibu na Huduma ya Polisi ya Haiti na maafisa wa kikosi cha Kimataifa cha kudumisha amani Haiti (MSS), maafisa wa polisi wa Kenya walitwaa miundombinu muhimu kama vile uwanja wa ndege, bandari na mapito makuu ya usafiri,” alisema Murkomen alipowatembelea maafisa hao nchini Haiti.

Aidha, kutokana na kujitolea kwa maafisa wa polisi wa Kenya kuhakikisha utulivu na usalama unadumishwa nchini Haiti, Murkomen alisema juhudi hizo zilizaa matunda huku zikiwezesha kufunguliwa tena kwa shule, hospitali na biashara.
“Walirejesha uwepo wa serikali katika maeneo ambayo hapo awali hayangefikiwa na kufanikisha kufunguliwa tena kwa shule, hospitali, na biashara,” alisema Waziri huyo.
Murkomen alidokeza kuwa mshikamano wa Kenya na Haiti utaendelea kudumu, licha ya kukamilika kwa operesheni hiyo huku akiwashukuru washirika wote kwenye operesheni hiyo waliojitolea kuhakikisha amani, utulivu na usalama unadumishwa.
Kikosi cha kwanza cha maafisa wa polisi wa Kenya cha maafisa 230, kiliwasili nchini Haiti mwezi Juni mwaka 2024, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha kubuniwa kwa kikosi cha kimataifa kukabiliana na magenge ya wahalifu nchini humo.