Naibu Rais wa Kenya Prof. kithure Kindiki ameelezea ufanisi mkubwa kutokana na mpango wa kidijitali kupitia vituo vya ICT kote nchini.
Akizungumza Jumanne katika Kongamano la Connected Africa Summit 2026 jijini Nairobi, Naibu huyo wa Rais alisema vituo 382 vya ICT hapa nchini, vimebuni nafasi 300,000 za ajira huku vituo vingine 400 vikiendelea kujengwa.
Kindiki alidokeza kuwa mpango huo ni nguzo kuu inayolenga kujenga miundomsingi muhimu ya kidijitali ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa muda mrefu wa Kenya.
Kwenye mkutano huo, Kindiki alizitaka nchi za Afrika kupitisha sera za mkakati wa umoja wa kidijitali, akisema ni muhimu kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya bara hili na kuhakikisha linakuwa mshindani wa kimataifa.
“Katika siku za usoni, ujumuishaji wa suluhu za ICT barani Afrika, ushirikiano kati ya sekta ya umma na ile ya kibinafsi kutafuta rasilimali za kifedha na za kibinadamu zinazohitajika kubuni utajiri kupitia teknolojia, zinasalia kuwa mkakati wa kiuchumi katika karne hii ya 21,” alisema kindiki.
Aliyasema hayo alipofungua rasmi mkutano huo wa 15 wa Connected Africa Summit 2026, kwa niaba ya Rais William Ruto.
Mkutano huo umewaleta pamoja Mawaziri na maafisa wa ngazi za juu kutoka mataifa 30.