Wachezaji watakaoondoka uwanjani kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa kuanzia kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, wataonyeshwa kadi nyekundu.
Bodi ya kimatifa ya shirikisho la kandanda ulimwenguni (IFAB), imepitisha sheria hiyo mpya katika kikao kilichofanyika mapema Jumatano mjini Vancouver,Canada.
Pia kocha atakayewashurutisha au kuwachochea wachezaji kuondoka uwanjani kupinga uamuzi wa refa ataonyeshwa kadi nyekundu.
Aidha, IFAB imesema kuwa wachezaji watakaozungumza na wenzao uwanjani wakiwa wamefunika midomo watapokea kadi nyekundu.
Sheria hizo mpya zitaanza kutumika kuanzia kwa fainali za Kombe la Dunia kati ya Juni 11 na Julai 19 mwaka huu, katika mataifa ya Canada,Mexico na Marekani.
Hatua hiyo inalenga kuleta nidhamu na kumaliza utundu kama ulioshuhudiwa wakati wa fainali ya AFCON Januari 18 mwaka huu wakati wachezaji wa Senegal, walipoondoka uwanjani baada ya kuamrishwa na kocha Pape Thiaw, wakicheza dhidi ya wenyeji Morocco.
Senegal waliteta kuhusu penati iliyopewa Morocco, hatua iliyosababisha kusitishwa kwa mchezo kwa zaidi ya dakika 10.