Rais William Ruto amesema mikakati iliyotekelezwa na serikali katika sekta ya kilimo, inaendelea kuzaa matunda, huku wakulima wakinakili mapato yaliyoimarika.
Akizungumza alipozuru kiwanda cha miwa cha Nzoia kaunti ya Bungoma, Ruto alisema ufanisi huo katika sekta ya kilimo umesababisha na hatua za kijasiri ambazo ni pamoja na kupunguza bei ya mbolea kutoka shilingi 7,000 hadi shilingi 2,500, kuondoa makundi ya wakiritimba na mageuzi katika usimamizi wa viwanda vya sukari.
“Katika sekta ya sukari, viwanda vinarejelea uzalishaji ulioimarika. Wakulima sasa wanalipwa ndani ya siku saba baada ya kuwasilishwa kwa miwa na wafanyakazi wanalipwa kwa wakati,” alisema Rais Ruto.
Alisema tangu serikali ya Kenya Kwanza ilipochukua usukani, mageuzi yametekelezwa katika sekta ya kilimo, ambayo yameimarisha utoshelevu wa chakula na kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.
“Taifa hili ni sharti lisonge mbele kwa kuzingatia mawazo bora, uongozi na lengo la taifa la pamoja,” alidokeza Rais Ruto.
Kwenye ziara hiyo, kiongozi huyo wa taifa alizindua ujenzi wa barabara ya kilomita 41 ya Bukembe-Nzoia Market-Mutomolo, katika kaunti ya Bungoma.