Wetang’ula awasihi wabunge kutanguliza majukumu ya kamati na bunge

Spila alisema hayo kwenye mkutano wa katikati ya muhula wa wabunge wa Bunge la Taifa unaoendelea mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ameeleza wasiwasi kuhusu hatua ya wabunge ya kukosa kuhudhuria vikao vya kamati mbalimbali za bunge mara kwa mara, akisema kuwa ukosefu wa akidi ni kikwazo kikubwa kwa shughuli za bunge.

Akizungumza kwenye mkutano wa katikati ya muhula wa wabunge wa bunge la taifa mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru, Spika alikumbusha wabunge kuhusu wajibu wao.

“Jukumu lenu kama wabunge sio tu kutimiza akidi kwa mikutano ya kamati, bali kushiriki kikamilifu katika mijadala kulingana na masharti yaliyowekwa,” alisisitiza Wetang’ula.

Alibainisha kuwa kamati ni kama injini za shughuli za bunge na hivyo wanachama wanapaswa kutoa kipaumbele kwa shughuli za kamati hizo.

Spika Wetang’ula alielezea kwamba viongozi wa kamati wanakumbwa na changamoto kubwa kutoka kwa wabunge wanaokosa kuhudhuria vikao.

“Hudhurieni mikutano kwa wakati ili kuwapa viongozi wa kamati na sekretarieti muda wa kutosha kuzingatia jinsi ya kushughulikia masuala mbele ya kamati na sio kuwaomba wabunge wahudhurie ili kuafiki akidi,” aliongeza kusema.

Hata hivyo, Spika alikiri kwamba baadhi ya wabunge wamekuwa wakihudhuria mikutano ya kamati kwa bidii na hatua hii inapaswa kuigwa na wenzao wanaojiepusha na mikutano hiyo.

Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah kwa upande wake alilalamikia hatua ya baadhi ya viongozi wa kamati ya kukosa kuhudhuria vikao vya bunge.

Aliongeza kuwa ni aibu kwamba Spika anapokuwa bungeni, anapowaita viongozi wa kamati kujibu maswali yaliyowasilishwa bungeni anapata hawapo.

Mwenyekiti wa kamati ya utangamano na fursa sawa Adan Yusuf Haji naye alilalamika kwamba viongozi wa bunge wanachukua muda mwingi kuwasilisha masuala yao bungeni.

Haji alisema kwa sababu hiyo, wanachukua muda ambao wengine wangetumia kuchangia mijadala kwenye vikao.

Mbunge wa Mandera Magharibi alimuomba Spika kuingilia kati wakati wa matukio kama haya ili kuhakikisha kwamba wabunge wanapata muda wa kutoa michango yao katika vikao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *