Naibu Gavana wa Meru Isaac Mutuma, ataapishwa siku ya Jumatatu Machi 17, 2025 kuwa Gavana wa Kaunti hiyo, baada ya Mahakama Kuu kushikilia hatua ya bunge la Senate la kuondolewa mamlakani kwa Gavana Kawira Mwangaza.
Kulingana na gazeti rasmi la serikali lililochapishwa siku ya Ijumaa na kutiwa saini na mwenyekiti wa kamati ya mpito ya afisi ya Gavana Martin Gitiye, Mutuma anatarajiwa kuapishwa katika uwanja wa Mwendantu mjini Meru kuanzia saa mbili unusu asubuhi.
Kwenye gazeti hilo rasmi la serikali, Gitiye pia alichapisha majina ya wanachama wa kamati ya muda, watakaoongoza hafla hiyo ya kumuapisha Mtuma..
Mnamo siku ya Ijumaa, Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye, alitupilia mbali ombi la Gavana Mwangaza lililotaka kufutilia mbali hatua ya bunge la Senate ya kumuondoa mamlakani.
Baadhi ya viongozi wa eneo la Meru, waliridhia uamuzi wa mahakama, wakiwa na matumaini kochokocho kuwa miradi ya maendeleo itawasilishwa kwa wakazi wa kaunti hiyo.