Polisi wavamia makazi ya Spika Among

Kundi la mawakili linadaiwa kuwasilisha malalamishi dhidi yake, kuhusiana na mali anayomiliki.

Marion Bosire
2 Min Read
Anita Among, Spika wa awali wa bunge la Uganda

Maafisa wa polisi wa vitengo mbali mbali, jana Jumamosi walivamia makazi ya mbunge wa kike wa Bukedea, Anita Annet Among, huko Nakasero, Kampala, Uganda, kufuatia tuhuma za ufisadi.

Oparesheni hiyo ya kushtukizia ilijiri siku chache tu baada ya Among, ambaye amekuwa akihudumu kama Spika, kuelekezwa na uongozi wa chama kwamba ajiondoe kwenye kinyang’anyiro cha Uspika wa bunge jipya.

Huku Polisi wakikosa kutoa taarifa rasmi kuhusiana na hatua yao ya kuvamia makazi ya Among, wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini Uganda wanahisi kwamba masaibu yake yanatokana na hali yake ya kutoelewana na uongozi wa chama cha NRM.

Baada ya wabunge wa bunge la 12 kuapishwa rasmi kuanza kazi Anita akiwa mmoja wao, ilitarajiwa kwamba mambo yatakuwa tu kawaida ambapo angewania tena wadhifa wa spika.

Marafiki wa Among ambaye ni mwanasiasa wa muda mrefu, wanahisi kwamba uvamizi wa makazi yake ni hatua inayolenga kumtishia kisiasa na wanamtia moyo wakimsihi asimame imara.

Ijumaa kitengo cha uchunguzi cha serikali ya Uganda, kilitangaza kwamba kinatayarisha malalamishi yaliyowasilishwa kuhusu mali ya Among, kufuatia ombi lililowasilishwa na kundi la mawakili.

Wawasilishaji wa malalamishi hayo wanahisi kwamba Among hajakuwa mkweli katika kutaja kiwango cha mali yake wakisema kuna uwezekano alitaja kiwango kidogo ikilinganishwa na mali anayomiliki.

Share This Article