Polisi wanasa kilo 315 za bangi kaunti ya Kilifi

Baada ya upekuzi wa kina, polisi walipata magunia mawili na nusu ya bangi ya thamani ya shilingi 9,465,000.

Tom Mathinji
1 Min Read
Polisi wanasa kilo 315 za bangi kaunti ya Kilifi.

Maafisa wa Polisi wamenasa kilo 315.5 za bangi katika eneo la Kuruwitu, Shariani, kaunti ya Kilifi.

Mihadarati hiyo ilinaswa baada ya maafisa hao kuwasili ili kumkamata mshukiwa wa uharibifu wa mali, ambaye alitoroka na kuacha nyuma bidhaa hiyo.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imesema operesheni hiyo ilitekelezwa na maafisa kutoka Kilifi Kusini, waliokuwa wakimwandama Martin Katana Charo almaarufu Ndume katika makao yake, ili wamtie nguvuni, lakini alikwepa kukamatwa alipotoroka kupitia dirishani.

“Maafisa hao kisha walihisi harufu ya bangi katika nyumba ya mshukiwa. Baada ya upekuzi wa kina, polisi walipata magunia mawili na nusu ya bangi ya thamani ya shilingi 9,465,000,” ilisema DCI.

Aidha, maafisa hao pia walipata magunia mawili ambayo hayakuwa na chochote, kitambulisho cha taifa cha mshukiwa huyo, na vifaa kadhaa vya upakiaji kuashiria eneo hilo hutumika kwa uhifadhi na upakiaji wa mihadarati hiyo.

Mihadarati hiyo ilichukuliwa na maafisa wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati, huku maafisa wakiendelea kumtafuta mshukiwa aliyetoroka.

TAGGED:
Share This Article