Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Brian Mundubile, amefunguliwa mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali, Mahakama Kuu ya nchi hiyo ikitarajiwa kuanza kusikiliza kesi ya uhaini dhidi yake.
Mundubile na washirika wake, wanatuhumiwa kupanga njama za kuipindua serikali kati ya mwezi Aprili na Agosti 2026.
Mundubile na mgombea mwenza kwenye Uchaguzi Mkuu Makebi Zulu, walikamatwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma za uhaini muda mfupi baada ya Uchaguzi wa Urais, waliodai uliibwa.
Rais Hakainde Hichilema alishinda uchaguzi huo na amekanusha madai ya kuwepo kwa udanganyifu wowote.
Kulingana na hati ya mashataka, Mundubile na mfanyabiashara mmoja walitoa fedha kwa ajili ya kuwapeleka watu watano nchini Urusi kupata mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kutekeleza mpango wa kuipindua serikali.
Wakili wa upande wa utetezi, Sakwiba Sikota, amesema mashtaka hayo hayana msingi na kwamba upande wa mashtaka unafanya uchunguzi wa kubahatisha ili kutafuta ushahidi wa kuwashtaki.
Sikota amesema kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mapema mwakani.
Awali, Mundubile alikanusha mashtaka hayo ya uhaini na kusema kuwa yanasukumwa na sababu za kisiasa.