Kenya imetia saini mkataba wa pili wa uhamishaji wa wafanyikazi na jimbo la New Brunwick nchini Canada.
Mkataba huo wa Maelewano ambao umejiri ndani ya mwezi mmoja na ule wa kwanza, unalenga kuweka msingi wa ushirikiano, mafunzo na uhamishaji wa wataalam kati ya Kenya na Canada.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Nairobi, Katibu wa idara ya Kazi na Maendeleo ya Ujuzi Shadrack Mwadime, alisema ushirikiano huo unaonyesha maslahi ya pamoja katika kukuza ujuzi na kupanga kazi kwa manufaa ya pande zote.
Mwadime alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Kenya, huku Canada ikiwakilishwa na Waziri wa Elimu, Mafunzo na Leba wa Mkoa wa New Brunwick Jean-Claude D’Amours.
Mkataba huo unatoa fursa ya ushirikiano katika utoaji mafunzo na utaalam ambao unafanikisha ukuaji wa ujuzi na mipango ya nguvukazi.
Wakati huo huo, mkataba huo unawezesha taasisi husika kushirikiana na washikadau kwa manufaa ya pamoja.