Rais Ruto: Serikali inawekeza shilingi bilioni 21 kaunti ya Kakamega

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto akutana na viongozi wa mashinani kaunti ya Kakamega, Novemba 1,2025.

Serikali inawekeza shilingi bilioni 21 katika miradi ya maendeleo kaunti ya Kakamega, ili kufanikisha ukuaji na kuhakikisha maendeleo sawa kote nchini. 

Akizungumza Jumamosi katika kaunti ya Kakamega, kiongozi wa nchi alisema uwekezaji huo unajumuisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa gharama ya kitita cha shilingi bilioni 14, ujenzi wa soko la kisasa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5, na ujenzi wa nyumba za malazi za wanafunzi wa elimu ya juu, kwa gharama ya shilingi bilioni mbili.

Aidha, Rais alisema serikali inazindua kiwanda cha dhahabu katika eneo la Ikolomani kitakachogharimu shilingi bilioni 1.5, kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wananufaika na mali asili katika kaunti hiyo.

“Tumezindua ujenzi wa barabara za kilomita 230 katika kaunti hii na kutenga shilingi bilioni 2.6 za kuunganisha umeme kwenye makazi ili kutimiza ajenda yetu ya upatikanaji wa nguzu za umeme,” alisema Rais Ruto.

Wakati huo huo, Rais alisema serikali tayari inaimarisha viwango vya uwanja wa ndege wa Kakamega kwa kuongeza urefu wa barabara ya ndege kutoka mita 900 hadi kilomita 1.2, na kuufanya uweze kuhudumia ndege kubwa kwa lengo la kufanya Kakamega kuwa kitovu cha kiuchumi.

Alisema serikali itakamilisha ujenzi wa uwanja wa Bukhungu kwa kitita cha shilingi bilioni 1.4, na hospitali ya rufaa na mafunzo ya kaunti ya Kakamega kwa shilingi bilioni 1.

Kulingana na Rais Ruto, miradi hiyo inalenga kuboresha maisha ya wakazi, kupanua upatikanaji wa fursa na kuhakikisha maendeleo sawa kote nchini.

Rais aliyasema hayo alipokutana na viongozi wa mashinani  wa kaunti ya Kakamega katika Ikulu ndogo ya Kakamega.

Website |  + posts
Share This Article