Mafarao watimuliwa Kombe la Dunia kishujaa na Argentina

Messi alisawazisha zikisalia dakika 6 mechi ikamilike kabla ya Ezno Fernandez kupachika la uongozi kwa mara ya kwanza.

Dismas Otuke
1 Min Read

Misri imewatoa mabingwa watetezi Argentina kijasho chembamba kabla ya kuaga kipute cha Kombe la Dunia Jumanne jioni baada ya kuzidiwa maarifa mabao 2-3 ugani Atlanta.

The Pharaohs walianza vyema mechi hiyo wakichukua uongozi dakika ya 15 kupitia kwa bao la kichwa lake Yasser Ibrahim.

Dakika sita baadaye, Argentina walipata fursa ya kurejea mchezoni kupitia kwa penalti iliyopigwa na nahodha Lionel Messi, ila ikapanguliwa na kipa Mostafa Shobeir na kudumisha uongozi huo kuelekea mapumzikoni.

Misri walirejea kipindi cha pili kwa matao ya juu wakiendeleza mashambulizi na nguvu mpya  na Mustafa Zico kutanua uongozi kwa goli la pili dakika ya 67.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Lionel Scaloni yalizaa matunda huku Argentina wakishambulia zaidi na Christian Romero akirejesha bao moja kunako dakika ya 79, akiunganisha pasi ya Messi.

Messi alisawazisha zikisalia dakika 6 mechi ikamilike kabla ya Ezno Fernandez kupachika la uongozi kwa mara ya kwanza.

Matokeo hayo yalizima matumaini ya Misri kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza huku Argentina wakijikokota kuelekea robo fainali.

Share This Article