Paraguay walifuzu kwa hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia kwa mara ya nne katika historia baada ya kuwatimua mabingwa mara nne Ujerumani kwa penalti 4-3 katika hatua ya 32 bora Jumatatu usiku.
Pambano hilo lililosakatwa katika uchanjaa wa Boston, Marekani lilishuhudia Paraguay wakiwabana Wajerumani kuanzia dakika za mwanzo huku Julio Enciso akiwaweka Paraguay uongozini katika dakika ya 42 baada ya kuunganisha pasi ya Matias Galarza.
Hata hivyo, Ujerumani walirejea mchezoni kwa bao la dakika ya 54 lake Kai Havertz, akiungisha krosi ya Florian Wirtz.
Timu zote zikifunga milango yao tokea hapo huku safu ya nyuma ya Paraguay, ikifanikiwa kuzima mashambulizi yote ya Ujerumani na kulazimu mechi kuelekea muda wa ziada.
Ilibidi penalti zichongwe ili kutenganisha timu hizo baada ya mshindi kukosekana ndani ya dakika 120, ambapo Paraguay walifunga 4 dhidi ya 3 za Wajerumani.
Paraguay watakumbana na mshindi kati ya Ufaransa na Uswidi katika raundi ya 16 bora.