Seneta wa Baringo William Cheptumo, ameaga dunia mapema Jumapili akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.
Kulingana na taarifa kutoka kwa familia, marehemu alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo kwa muda, akitibiwa ugonjwa ambao hawakuufichua, na aliruhusiwa kuondoka wiki jana.
Hata hivyo, hali yake ilidorora zaidi, na alirejeshwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Cheptumo aliyekuwa na umri wa miaka 57, alihudumu kama mbunge wa Baringo Kaskazini kati ya mwaka 2008 na 2013, kabla ya kuchaguliwa Seneta mwaka 2022 kwa tiketi ya chama cha UDA baada ya kumshinda Gideon Moi.
Marehemu pia alikuwa amehitimu kwa shahada ya uanasheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na alilimiki kampuni ya mawakili iliyokuwa ikiwakilisha benki kuu ya Kenya.
Rais William Ruto ametoa risala za rambirambi kwa familia, akimtaja marehemu kuwa kiongozi aliyejitolea kuitumikia nchini kwa hali na mali.