Beatrice Wangare ambaye anachunguzwa kutokana na kifo kinachokumbwa na utata cha Daktari Job Obwaka, atazuiliwa kwa siku 10 zaidi kwenye korokoro za polisi kutoa fursa kwa uchunguzi zaidi kufanywa.
Viongozi wa mashtaka walitoa ombi kwa hakimu wa mahakama ya Kibera Babra Akinyi kuagiza Wangare aendelee kuzuiliwa huku wakifanya uchunguzi zaidi.
Wangare alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na Dkt. Obwaka katika eneo la Kitengela kabla yake kupelekwa kwenye hospitali hiyo ya Nairobi ambako ilithibitishwa kuwa alikuwa amefariki.
Mshukiwa huyo alikamatwa tarehe mosi mwezi huu kufuatia kifo cha Dkt. Job Obwaka nyumbani kwake katika mtaa wa Milimani huko Kitengela.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya sajini Rhoda Nzioka, Dkt. Obwaka alisafiri kwa gari lake kutoka Nairobi hadi eneo la Kitengela ambako alikutana na Wangare siku hiyo aliyemwendea katika jumba moja la kibiashara kabla ya kuandamana naye hadi nyumbani kwake.