Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amewamiminia sifa wanachama wa Baraza la Mawaziri wanaoondoka, kwenye dhifa iliyoandaliwa katika Ikulu ya Rais Jijini Entebe.
Aliwapogeza kwa huduma walizotoa na mchango wao mkubwa katika kufanikisha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Museveni alisifu Baraza hilo la Mawaziri kwa jukumu lake la kihistoria katika kuimarisha nchi hiyo hadi kiwango cha mapato ya wastani, akidokeza kuwa hatua hiyo inaashiria juhudi za pamoja, nidhamu na kujitolea mhanga.
Wakati huo huo, Rais huyo alitambua jukumu la wananchama hao kwenye mchakato wa uchaguzi wa hivi punde, akitaja matokeo hayo kama mafanikio ya pamoja, huku akielezea imani na ukuaji endelevu wa kiuchumi katika muhula wake wa uongozi unaofuata.
Kupitia ukurasa wake wa X, Rais Museveni alisisitiza haja ya kuzingatia uongozi wenye uadilifu, akitoa wito wa uwajibikaji na uzalendo katika utumishi wa umma.
Rais Museveni mwenye umri wa miaka 81, alichaguliwa tena kuiongoza Uganda, kwenye Uchaguzi Mkuu ulioandaliwa mwezi Januari 2026, akipata asilimia 71.65 ya kura zote zilizopigwa.