NPS yaomboleza kifo cha polisi wa Kenya nchini Haiti

Martin Mwanje
2 Min Read
Douglas Kanja (katikati) - Inspekta Mkuu wa Polisi

Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) imetuma risala za rambirambi kwa familia ya polisi wa Kenya aliyefariki wakati wa operesheni ya usalama nchini Haiti. 

Operesheni hiyo ilikuwa ikitekelezwa na timu ya usalama ya Kikosi cha Kimataifa cha Kudumisha Amani nchini Haiti (MSS) jana Jumapili wakati timu hiyo iliposhambuliwa na magenge ya wahalifu katika eneo la SÉGUR – SAVIEN na afisa huyo kujeruhiwa.

Kisha afisa huyo alifariki baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kusafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya Aspen Level 2 kwa matibabu.

Huyo ni afisa wa kwanza kufariki tangu maafisa wa polisi wa Kenya walipopelekwa kudumisha amani nchini Haiti.

Kupitia kwa msemaji wa polisi Muchiri Nyaga, idara hiyo inasema familia ya afisa huyo imetaarifiwa kuhusiana na kifo chake.

“Afisa huyo alipata majeraha ya risasi na kukimbizwa hospitalini, na kwa bahati mbaya alifariki kutokana na majeraha hayo,” alisema Nyaga kupitia taarifa.

“NPS inatuma risala zake za dhati za rambirambi kwa familia na marafiki wa polisi aliyefariki na kuwahakishia uungaji mkono wetu usiyoyumba wakati wa kipindi hiki kigumu.”

Nyaga akiongeza kuwa MSS kwa ushirikiano na Polisi wa Taifa wa Haiti (HNP) wanafanya kazi sako kwa bako kurejesha amani nchini humo.

Wiki chache zilizopita, kundi la nne la polisi wa Kenya liliwasili nchini Haiti kwa misheni ya kulinda amani.

Polisi hao ambao walijiunga na MSS, waliondoka nchini mapema mwezi huu kwa operesheni hiyo.

Kundi hilo la nne la polisi wa Kenya kwenda nchini Haiti, liliwajumuisha wanawake 24 kati ya maafisa 144 wa usalama, kwa lengo la na kushirikiana na wenzao walio Haiti kudumisha usalama.

Polisi hao walipokelewa na maafisa wakuu wa serikali ya mpito nchini Haiti, akiwemo Rais Leslie Voltaire na Kamanda wa MSS Godfrey Otunge.

 

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article