Kenya yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake Afrika Kusini

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya nchini watakiwa kuchukua tahadhari za kiusalama.

Raia wa Kenya wanaoishi Afrika Kusini w ametakiwa kuwa waangalifu, kufuatia maadamano yanayoshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za taifa hilo yanayowalenga raia wa kigeni.

Kupitia kwa taarifa kwenye ukurasa wa X, ubalozi wa Kenya Afrika Kusini umewasihi wakenya kuepuka maeneo ya maandamano na kuzingatia ushauri unaotolewa na utawala wa taifa hilo.

“Ubalozi wa Kenya Pretoria unawashauri raia wote wa Kenya wanaoishi Afrika Kusini kuchukua tahadhari kutokana na maandamano yanayoshuhudiwa katika sehemu kadhaa za nchi hiyo yanayowalenga raia wa kigeni,” ilisema taarifa ya ubalozi huo.

Wakati huo huo, ubalozi huo umewashauri wakenya kubeba vitambulisho vyao na stakabadhi zingine muhimu kila wakati.

Aidha, raia wa Kenya wameshauriwa kuripoti visa vyovyote kwa Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini na kwenye ubalozi wa Kenya nchini humo kwa usaidizi iwapo kutatokea hali ya dharura.

Ubalozi huo ulisema uko tayari kuwasaidia raia wake, huku ukitoa nambari za mawasiliano ambazo ni +27 (012 362 2249), +27 (076 177 2675), au barua pepe info@kenya.org.za.

Share This Article