Waliosababisha kifo cha Rachel Wandeto kuwajibishwa, aapa Rais Ruto

Wandeto ni mwanamke aliyesifika mitandaoni kwa kujichora picha ya Rais Ruto kwenye mwili wake, na alifariki mapema Jumatatu wiki hii.

Martin Mwanje
2 Min Read
Rachel Wandeto aliyeripotiwa kukumbana na mauti kufuatia msimamo wake wa kisiasa

Rais William Ruto ameapa kuhakikisha waliohusika katika mauaji ya Rachel Wandeto wanakamatwa na kuwajibishwa kutokana na kitendo chao cha kikatili. 

Ruto pia amekemea uenezaji wa chuki kwa misingi ya kikabila akisema mienendo kama hiyo haitakubaliwa nchini kamwe.

“Maisha ya Rachel Wandeto hayatatoweka bila kuwajibishwa. Nyinyi mliowaita wengine wasaliti mpaka Mama Rachel Wandeto ameuawa kwa sababu ya chuki yenu, kwa sababu ya ukabila wenu, kwa sababu ya kuwaita Wakenya wengine kwamba ni wasaliti, siku moja mtajibu,” alionya Ruto.

“Kenya hii, hatuwezi kukubali, hatuwezi kuwaruhusu mtuuzie ukabila, mtuuzie chuki, mtuuzie blackmail.”

Kiongozi wa nchi aliyasema hayo alipohutubia hadhira katika eneo la Mama Ngina Drive, kaunti ya Mombasa leo Alhamisi.

Alitumia fursa hiyo kuupuzilia mbali upinzani aliyosema hauna ajenda yoyote ya kuwanufaisha Wakenya kamwe.

“Kwa wale ambao hamna maono wala ajenda kwa taifa letu, watu wasiokuwa na mpango kwa taifa letu, hamtagawanya taifa letu kwa kutumia ukabila, Hamtangawanya nchi yetu kwa kutumia chuki. Hiyo mnafanya, chuki mnayoeneza, nataka kuwaambia, siku moja mtawajibikia ukabila mnaoeneza nchini Kenya.”

Wandeto ni mwanamke aliyesifika mitandaoni kwa kujichora picha ya Rais Ruto katika mwili wake, na  alifariki mapema Jumatatu wiki hii.

Wandeto ambaye ni mkazi wa Mwiki, alilazwa Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta mwishoni mwa wiki jana baada ya kuchomwa na watu wasiojulikana.

Yamkini marehemu alipata majeraha ya moto ya asilimia 70, baada ya kuteketezwa na wanaume watatu wasiojulikana.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alimtembelea Wandeto hospitalini Jumapili jioni huku akilaani shambulizi hilo.

Polisi wameanzisha msako wa waliohusika katika mauaji hayo huku mtu mmoja akiripotiwa kukamatwa wakati uchunguzi ukiendelea

Share This Article