Ruto aanza ziara ya siku tano eneo la Pwani

Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto atatoa hatimiliki kwa wakazi wa eneo hilo huku akizindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ameanza ziara ya maendeleo ya siku tano eneo la Pwani, punde baada ya kuwasili nchini kutoka kwenye ziara ya siku mbili nchini Kazakhstan. 

Ziara hiyo ilianza kwa Rais Ruto kuelekea eneo la Mama Ngina Drive, kaunti ya Mombasa ili kutoa hatimiliki za ardhi kwa wakazi.

Hatimiliki hizo zitatolewa kwa kaunti zote sita za eneo hilo katika jitihada za kukabili tatizo sugu la ardhi ambalo limekuwa mwiba kwa wakazi kwa muda mrefu.

Magavana Abdullswamad Sheriff Nassir wa Mombasa na Gideon Mung’aro wa Kilifi ni miongoni mwa viongozi waliomlaki Rais Ruto.

Wengine ni Mawaziri Hasan Joho wa Madini na Salim Mvurya wa Michezo.

Akiwahutubia wakazi, Gavana Mung’aro aliusifia utawala wa Kenya Kwanza kwa miradi ya maendeleo unaotekeleza eneo hilo na kuwataka wakazi kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili wakati wa uchaguzi mkuu mwakani.

Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto atakabidhi miradi ya maendeleo iliyokamilika kwa uongozi wa eneo la Pwani wakati akikagua miradi inayoendelea.

Miradi hiyo inajumuisha uunganishaji wa umeme, masoko na ujenzi wa barabara miongoni mwa mingine.

 

 

 

Share This Article