Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu Mipaka Nchini, IEBC imefanikiwa kusajili wapiga kura wapya milioni 1,876,274 takwimu za hadi Aprili 23, 2026, chini ya mpango ulioimarishwa wa usajili wa wapiga kura.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari ya Aprili 24, 2026, tume hiyo ilielezea kwamba idadi hiyo ya wapiga kura inajumuisha ongezeko la wapiga kura 505,344 tangu Aprili 17, ilipotoa takwimu.
IEBC ilisema kwamba wakenya watafanya uchaguzi mkuu Agosti 10, 2027 ambapo watachagua viongozi wa nyadhifa 6.
Wakenya waliotimiza umri wa kupiga kura na ambao bado hawajasajiliwa kuwa wapiga kura watumie fursa hii ya siku zilizosalia chini ya mpango ulioimarishwa wa usajili.
“Kadri zoezi la usajili ulioimarishwa linakaribia kuhitimishwa, tunawahimiza wapiga kura wote wanaostahili ambao bado hawajajisajili kuchangamkia fursa hii,” taarifa hiyo ilisema, ikiongeza kuwa usajili wa wapiga kura ni muhimu katika kushiriki mchakato wa kidemokrasia.
Kulingana na taarifa hiyo, wapiga kura 159,410 wameomba kuhamishiwa vituo tofauti vya kupigia kura, huku watu 2,817 wakisasisha au kurekebisha taarifa zao za usajili.
IEBC pia ilithibitisha tena haki ya kikatiba ya kila Mkenya kushiriki uchaguzi, kama ilivyoainishwa chini ya Ibara ya 38, ambayo inahakikisha haki za kisiasa ikiwa ni pamoja na kupiga kura na kuwania nyadhifa za umma.